Advertisements
RSS

China kusaidia Afrika dola za Marekani bil. 20‏

19 Jul

Beijing

Bernard Membe – Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa

SERIKALI ya Jamhuri ya Watu wa China, imetangaza kutoa msaada wa Dola za Marekani bilioni 20 kwa ajili ya kusaidia nchi za Afrika katika miaka mitatu ijayo.

Fedha hizo kwa mujibu wa Rais Hu Jintao, zitakwenda kusaidia maeneo ya kilimo, miundombinu, uzalishaji bidhaa na wajasiriamali wa kati na wadogo.

Rais Hu alitangaza msaada huo jana mjini hapa wakati akifungua Mkutano wa Tano wa Mawaziri wa Ushirikiano kati ya China na Afrika (FOCAC), unaofanyika kwa siku mbili.

 

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe na Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Gregory Teu wanaiwakilisha Tanzania katika mkutano huu.  Baloziwa Tanzania nchini China, Philip Marmo pia alihudhuria ufunguzi huo.

Rais Hu alisema China itaendelea kuongeza misaada yake kwa Afrika ili kuleta maendeleo kwa watu wa Afrika. “China itajenga vituo vingi vya kisasa vya mfano vya teknolojia ya kilimo ili kuisaidia Afrika katika kuongeza uzalishaji wa chakula.

“China itatekeleza Programu ya Vipaji vya Kiafrika kwa kuwafunza maofisa 30,000 wa Afrika katika sekta mbalimbali, kutoa udhamini wa masomo kwa maofisa wa Serikali 18,000 na kujenga vituo vya utamaduni na vyuo vya ufundi katika nchi mbalimbali za Afrika,” alisema Rais Hu.

Alisema kuwa China itapeleka Afrika wataalamu 1,500 wa afya katika nchi za Afrika, huku pia ikizisaidia nchi za Afrika katika miundombinu ya hali ya hewa na uhifadhi wa misitu.

Kwa mujibu wa Rais Hu, eneo jingine ambalo China itatilia mkazo ni ushirikiano kati ya nchi za Afrika na katika hili, itasaidia kuboresha miundombinu ili kusaidia watu wa vijijini

pamoja na kusaidia viwanda na udhibiti wa forodha kwa bidhaa zinazoingia Afrika.

“Kutakuwa pia na ushirikiano wa pamoja kati ya watu wa China na Afrika ili wanufaike na ushirikiano huu. Tutaanzisha vituo vya habari kwa ajili ya kubadilishana uzoefu na kujenga uhusiano katika tamaduni zetu.

“Pia kutakuwa na programu za pamoja za utafiti 100 zitakazohusisha wanazuoni,” alisema Rais Hun na kushangiliwa na viongozi mbalimbali wakiwamo marais sita wa Afrika wakiongozwa na Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika, Rais Yaya Boyi wa Benin.

Alilitaja eneo jingine ambalo China italitilia mkazo ni kuimarisha ushirikiano na AU na nchi za Afrika katika suala la amani na usalama na kutoa msaada wa kifedha kwa vikosi vya kulinda amani Afrika na kuboresha Jeshi la Akiba la Afrika na kuwafunza maofisa wengi zaidi kuhusu amani na usalama.

Alisema China inaamini maeneo ambayo yanapaswa kutiliwa mkazo ni miundombinu, kilimo, fedha, utengenezaji bidhaa, teknolojia na biashara.

Afrika ndio eneo ambalo China ina uwekezaji mkubwa kwa sasa duniani, ambapo mwaka jana pekee, nchi za Afrika na China zilifanya biashara ya Dola za Marekani bilioni 163.3.

Aidha, uwekezaji wa moja kwa moja wa China kwa Afrika mwaka jana ulikuwa Dola za Marekani bilioni 15 katika nchi 50 za bara hili ambalo kwa pamoja na China, lina idadi ya watu ambayo ni theluthi moja ya idadi ya watu wote duniani kwa sasa.

Ushirikiano kati ya China na Afrika ulianzishwa rasmi mwaka 2000, na umekuwa ukiimarika na Afrika imekuwa ikijivunia kupata misaada mingi kutoka kwa mshirika wake huyo mpya wa maendeleo siku za karibuni.

Akizungumza katika ufunguzi huo, Rais Jacob Zuma wa Afrika Kusini ambayo nchi yake imepokea kiti cha uenyekiti wenza kutoka kwa Misri, alisema ushirikiano wao huo na China ni tofauti na ule wa nchi za Ulaya.

Hata hivyo, alisema pamoja na ushirikiano huo kuzaa matunda mengi na Afrika kufaidika, bado bara hili linakabiliwa na changamoto za miundombinu, teknolojia ya mawasiliano na nishati.

Advertisements
 

Tags: , , , , , , , , ,

One response to “China kusaidia Afrika dola za Marekani bil. 20‏

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out / Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out / Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out / Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out / Change )

Connecting to %s

 
%d bloggers like this: