Advertisements
RSS

Viwango Vikubwa Vya Riba za Mikopo Zinazotozwa na Mabenki ya Biashara ni Changamoto Kwa Sekta ya Fedha Nchini

27 Jun

WAZIRI Mkuu, Mizengo Pinda amesema, viwango vikubwa vya riba kwenye mikopo katika benki za biashara ikilinganishwa na riba ndogo inayolipwa kwa amana ni changamoto kubwa katika sekta ya fedha nchini.
 
“Serikali inazitambua changamoto hizo na tayari mikakati inaandaliwa kukabiliana nazo hususan kuanzisha dirisha la kilimo katika Benki ya Rasilimali Tanzania na kukamilisha mchakato wa kuanzisha Benki ya Maendeleo ya kilimo” amesema Pinda bungeni mjini Dodoma wakati anasoma hotuba kuhusu mapitio na mwelekeo wa kazi za Serikali na makadirio ya matumizi ya fedha ya ofisi ya Waziri Mkuu na Ofisi ya Bunge kwa mwaka 2012/2013.
 
Amesema, Serikali inaendelea kuboresha mazingira ya uwekezaji pamoja, kuanzisha mfumo wa kuwatambua wakopaji na imetoa msukumo wa uanzishaji wa huduma za kifedha kupitia Vyama vya Kuweka na Kukopa (SACCOS).
 
Kwa mujibu wa Pinda, hadi sasa kuna jumla ya SACCOS 5,346 na vimetoa mikopo yenye thamani ya shilingi bilioni 627.2.
 
Amesema, Serikali kupitia Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi imeendelea kusimamia na kuratibu utekelezaji wa Sera ya Taifa ya Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi ya mwaka 2004 kupitia programu na mifuko mbalimbali.
 
“Hadi kufikia mwezi Aprili 2012, Mfuko wa Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi umetoa mikopo yenye thamani ya shilingi bilioni 7.3 kwa wajasiriamali 7,187 katika mikoa ya Dodoma, Lindi, Manyara, Mtwara, Pwani, Rukwa, Ruvuma, Singida na Tanga” amesema.
 
Kwa mujibu wa Waziri Mkuu, sehemu kubwa ya mikopo iliyotolewa ilitumika kugharamia shughuli za kilimo ikijumuisha ununuzi wa pembejeo na zana za kisasa za kilimo na umwagiliaji.
 
“Serikali imeendelea kuweka mazingira wezeshi kwa sekta binafsi ili iweze kushiriki kikamilifu katika shughuli za uzalishaji mali na kufanya biashara na hatimaye kuwa injini ya ukuaji wa uchumi”amesema.
 
Amesema, Serikali inasimamia utekelezaji wa mpango kazi wa kuboresha mazingira  ya biashara na uwekezaji nchini wenye lengo la kurekebisha mifumo iliyopo ili kupunguza gharama za kufanya biashara na kuwekeza nchini.
 
“Hatua zilizochukuliwa ni pamoja na uanzishaji wa kituo kimoja cha utoaji wa huduma kwenye Bandari ya Dar es Salaam, ambapo muda wa mizigo kukaa bandarini umepungua kutoka wastani wa siku 25 mwaka 2009 hadi kufikia wastani wa siku 9 mwezi Mei 2012” amesema.
 
Pinda pia amewaeleza wabunge kuwa, katika mwaka 2011/2012, Serikali imefanya juhudi kubwa za kuhamasisha na kuvutia wawekezaji wa ndani na nje na kwamba, Kituo cha Uwekezeji (TIC) kilisajili jumla ya miradi 681 yenye thamani ya shilingi trilioni 11.6, na ilitoa fursa 89,803 ya ajira.
 
Amewaeleza wabunge kuwa, miradi 356, sawa na asilimia 52.3 ni ya wawekezaji wa ndani, miradi 166, sawa na asilimia 24.4 ni ya ubia kati ya wawekezaji wa ndani na nje na miradi 159, sawa na asilimia 23.3 ni ya wawekezaji wa nje.
 
“Mitaji ya moja kwa moja kwa moja ya wawekezaji wa nje (FDI), iliyoingizwa nchini imeongezeka kutoka shilingi bilioni 681.2 mwaka 2010 hadi trilioni 1.3 mwaka 2011” amesema.
 
Pinda amesema, Serikali imeanza kuona matunda mazuri yaliyotokana na ushirikiano kati ya wawekezaji wakubwa na wakulima wadogo katika kuongeza uzalishaji na tija.
 
“Maandalizi ya kuainisha miradi itakayotekelezwa na wawekezaji wa ndani na nje katika ukanda wa SAGGOT yameanza. Kutokana na ukubwa wa ukanda huo wa kilimo, miradi itakayoainishwa itatekelezwa kwa mfumo wa wa kongano (clusters) ambapo wakulima wadogo watashirikishwa na wawekezaji wakubwa kuendeleza kilimo”amesema.
 
Waziri Mkuu ametoa wito kwa Watanzania kuona uwekezaji mkubwa katika kilimo kuwa ni fursa muhimu ya kuongeza uzalishaji na tija.
 
“Jambo la msingi ni kuhakikisha kwamba, maslahi ya wakulima wadogo yanalindwa kwa kuwekeana mikataba mizuri na kufuatilia utekelezaji wake. Ni imani yangu kwamba, tukiitumia vizuri ardhi yenye rutuba tuliyonayo tutaweza kuongeza ukuaji kwenye sekta ya kilimo ambayo ni tegemeo kwa Watanzania wengi na hatimaye kupunguza umasikini wa kipato” amesema.
 
Pinda amesema, ushirikiano baina ya Serikali na sekta binafsi ni nguzo muhimu ya kuleta mapinduzi ya kilimo, na kwamba, katika kipindi cha mwaka 2011/2012, Serikali iliimarisha upatikanaji wa pembejeo za kilimo hasa mbolea, mbegu bora na daza za mimea.
 
“Serikali inatambua kuwa, mkakati wa kuhimiza kilimo cha kisasa kinachotumia kanuni bora za kilimo, zana za kisasa na msukumo kwenye kilimo cha umwagiliaji ndiyo njia ya uhakika ya kuongeza uzalishaji na tija katika kilimo” amesema.

Posted by MJ

Advertisements
 

Tags: , , , , , , ,

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out / Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out / Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out / Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out / Change )

Connecting to %s

 
%d bloggers like this: