Advertisements
RSS

Kutoka Bungeni: Misamaha ya Kodi Kupunguzwa

19 Jun

Dodoma, Tanzania

 

WIZARA ya Fedha imesema, Serikali ina lengo la kupunguza misamaha ya kodi ili isizidi asilimia moja ya pato la taifa.

Naibu wa Fedha Ms.Saada Mkuya,Mb.

Naibu wa Fedha Ms.Saada Mkuya,Mb.

 

Naibu Waziri wa Fedha, Saada Mkuya Salum ameliambia Bunge mjini Dodoma kuwa, Serikali inaendelea kupitia baadhi ya sheria za misamaha ya kodi ili kuangalia kama bado zina manufaa kwa umma.

 

Amesema, ili kutimiza azma hiyo, Mamlaka ya Mapato (TRA) kupitia mfuko wa dhamana wa ushauri wa sera na usimamizi wa kodi ulioanzishwa na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) inafanya uchambuzi wa kina wa kuangalia sheria na kanuni za misamaha ya kodi.

 

Kwa mujibu wa kiongozi huyo wa Serikali, uchambuzi huo utaleta mapendekezo ya kuiondoa misamaha yote isiyo na maslahi na tija kwa taifa.

 

Salum amesema, mwaka ujao wa fedha, Serikali imechukua hatua za kurekebisha sheria mbalimbali za kodi kwa nia ya kupunguza misamaha na kuzuia mianya ya ukwepaji kodi.

 

Alikuwa akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalumu Amina Abdulla Amour (CUF) aliyetaka kufahamu ni lini Serikali itapunguza misamaha yakodi hadi kufikia chini ya asilimia moja ya pato la taifa kutokana na kuwa kero kwa muda mrefu kwa taifa kukosa fedha na mapato kwa ajili ya maendeleo.

 

“Sisi pale wizarani tumeamua kulivalia njuga suala hili, tutaifanya kazi hiyo na tunaomba tupewe muda kwani jambo hili haliwezi kufanyika kwa mara moja,” alisema.

 

Wakati huo huo, Salum alisema Benki ya Wanawake inaweza kushiriki katika mpango wa kukopesha na kusimamia fedha za mabilioni ya Rais endapo inahitaji kufanya hivyo na taasisi zingine za fedha ambazo zimekidhi vigezo vilivyowekwa.

 

Alitaja vigezo hivyo kuwa ni pamoja na uwezo wa kuhudumia vijijini, kuwa na mizani nzuri za hesabu na uzoefu katika kuhudumia wajasiriamali wadogo.

 

Alisisitiza kuwa walengwa wa mfuko wa mabilioni ya Rais ni vijana, wazee, wanawake vijijini na mijini ambao wanafanya shughuli katika kuhudumia wajasiriamali wadogo.

 

Alikuwa akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalumu Faida Mohamed Bakar (CUF) ambaye alihoji kama Serikali inakubaliana naye kwamba sasa ni wakati muafaka wa kuhamisha fedha za mkopo wa mabilioni ya Kikwete na kutumika katika Benki ya Wanawake ili wananchi wapate mikopo.

 

Wakati huohuo, Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Fedha na Uchumi, imeafiki maeneo mengi ya kodi na tozo mbalimbali yaliyopendekezwa na Serikali kufanyiwa marekebisho, lakini ikasisitiza umuhimu wa nidhamu ya matumizi ya Serikali na uwezo wa kuongeza mapato.

 

Mbali na hayo, Kamati hiyo ilieleza kutoridhishwa na Serikali katika kasi ya kushughulikia misamaha ya kodi.

 

“Kamati inaishauri Serikali kuonesha dhamira ya kweli kufanikisha lengo hilo (la kuimarisha taratibu za kukusanya mapato pamoja na kupunguza misamaha ya kodi) na kutoa taarifa ya utekelezaji mbele ya Kamati Januari 2013,” amesema Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Andrew Chenge.

 

Chenge alikuwa anawasilisha taarifa ya Kamati yake kuhusu hali ya uchumi wa Taifa kwa mwaka 2011 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa mwaka 2012/13 pamoja na tathimini ya utekelezaji wa Bajeti ya Serikali kwa mwaka 2011/12 na mapendekezo ya mapato na matumizi ya Serikali kwa 2012/13.

 

“Kamati inaendelea kushauri kwamba Serikali iachane na mtindo wa kuibua matumizi mapya yasiyo ya dharura ambayo hayakuidhinishwa na Bunge wakati wa utekelezaji wa bajeti”

 

“Mtindo huo unavuruga bajeti na kupunguza uwezo wa kutoa fedha za matumizi mengineyo (OC) na matumizi ya maendeleo kama ilivyokusudiwa. Kamati inasisitiza umuhimu wa Serikali kubana matumizi kwa kupunguza matumizi yasiyo ya lazima,” amesema Chenge.

Advertisements
 
Leave a comment

Posted by on June 19, 2012 in Tanzania News

 

Tags: , , , , , , ,

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out / Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out / Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out / Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out / Change )

Connecting to %s

 
%d bloggers like this: