Advertisements
RSS

Mbunge Wa CCM Kuipinga Bajeti

17 Jun

Dodoma, Tanzania – Mwandishi wa MF Blog

MBUNGE wa Kisesa, Luhaga Mpina (CCM) ameapa kuipinga bajeti ya Serikali iliyowasilishwa bungeni mjini Dodoma, kwa maelezo kwamba imejaa ulaji wa wakubwa kupitia posho, warsha na safari zao za nje huku mamilioni ya Watanzania masikini wakifa kwa kukosa matibabu.

Amewaeleza waandishi wa habari kuwa, bajeti hiyo inakiuka azimio la Bunge kwamba kwa kila mwaka wa fedha angalau asilimia 35 itengwe kwa ajili ya miradi ya maendeleo na fedha za matumizi ya kawaida ziwe asilimia 65.

Lakini Mpina ambaye pia ni mjumbe wa Kamati ya Bunge ya Fedha na Uchumi alisema bajeti iliyowasilishwa na Waziri wa Fedha, Dk William Mgimwa, waliipinga kuanzia kwenye Kamati ya Fedha na kuishauri Serikali iibomoe, lakini hawakufanya hivyo.

Mbunge huyo amesema, yuko tayari kufukuzwa CCM akitetea fedha zaidi zitengwe kwa ajili ya miradi ya maendeleo, kwani warsha, sherehe, ununuzi wa samani, magari ya kifahari unaweza kupunguzwa au kuahirishwa ili kuwapa Watanzania maisha bora.

“Hiki ninachofanya si usaliti kwa chama, kwani ninachotetea ni kukisaidia chama chetu kiweze kutekeleza miradi yenye manufaa kwa wananchi na si kutenga fedha nyingi kwa posho na sherehe,” alisema Mbunge huyo.

Akichambua bajeti hiyo, Mpina alisema katika azimio la Bunge iliazimiwa kitengwe kiasi kisichopungua Sh trilioni 2.7 kutoka mapato ya ndani na zielekezwe kutekeleza mpango huo.

“Hivyo bajeti ambayo imewasilishwa na waziri si sahihi kwa mujibu wa mpango wa maelekezo ya Bunge,” alisema.

Akitoa mfano wa ulaji huo, Mbunge huyo alisema mafungu nane tu ya Wizara ya Nishati na Madini na  Fedha yameongezwa kiasi cha Sh bilioni 4.8 kwa ajili ya posho na safari za ndani na nje ya nchi, wakati fedha hizo zingepunguzwa na kuelekezwa kwenye miradi ya maendeleo.

Alisisitiza kuwa kitendo cha Serikali kutenga Sh trilioni 2.2 badala ya Sh trilioni 2.7 ambayo ni tofauti ya Sh bilioni 500 kugharimia miradi iliyoainishwa katika mpango huo,  kumesababisha miradi mingi kutengewa fedha kidogo na mingine mingi kukosa fedha kabisa, hali ambayo alidai inazorotesha utekelezaji na maana ya kuwa na mpango.

Mpina alisema kibaya zaidi, katika bajeti hiyo mapato ya ndani yameongezeka hadi Sh trilioni 1.5 huku matumizi ya kawaida yakipanda hadi Sh trilioni 1.9 wakati fedha za maendeleo zikipungua na kuwa Sh bilioni 397.8 ikilinganishwa na mwaka wa fedha wa 2011/12.

“Hapa inajidhihirisha kuwa Serikali haina nia ya dhati ya kupunguza matumizi ya kawaida,” alisema Mpina. Alisema kwa kipindi kirefu, imekuwa ikiahidi kupunguza matumizi ya kawaida ili kuongeza kasi ya utoaji huduma na uwekezaji katika sekta zinazokuza uchumi na kupunguza umasikini; lakini hivi sasa pato kuu la Taifa linatumika kuendesha Serikali.

Mpina alisema wakati Serikali ikiendekeza matumizi makubwa yasiyo na tija, Watanzania wanakufa kwa kukosa huduma za tiba, dawa, waganga, maji safi na salama, elimu bora kutokana na upungufu mkubwa wa madarasa, nyumba za walimu, vifaa vya kufundishia na maabara.

Pia miundombinu mibovu ya barabara, umeme na reli, ukosefu wa viwanda vya kuongeza thamani kunakosababisha wakulima kuuza mazao yao kwa bei ndogo, hasa pamba, mkonge, korosho na mifugo.

Alisema mpango wa maendeleo ni mkataba kati ya wananchi na Serikali, lazima wabunge ambao ni wawakilishi wa wananchi waulinde kwa nguvu zote na kwa gharama yoyote.

Alisema kama Serikali ilipata fedha za kufidia benki na wafanyabiashara walioathirika na mtikisiko wa uchumi kwa jumla ya Sh trilioni 1.7 “iweje leo ishindwe kupata Sh bilioni 500 kugharimia yaliyoainishwa katika mpango wa maendeleo?”

Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Fedha na Uchumi, Andrew Chenge alisema ingawa Waziri wa Fedha ameanza kwa mwelekeo mzuri, lakini matumizi ya kawaida ya Serikali yanapaswa kugharimiwa na fedha za ndani.

Mbali ya kusisitiza bajeti ya maendeleo iongezwe hadi asilimia 35, amesema kama Watanzania wanataka uchumi ukue na kuondoka na umasikini, lazima kilimo kibadilishwe na kiwe chenye tija.

“Mwelekeo mzuri, wameanza vizuri,” alisema Chenge ambaye pia ni Mbunge wa Bariadi Magharibi (CCM) aliyepata kuwa Waziri katika Awamu ya Nne.

Mwenyekiti huyo aliyechaguliwa hivi karibuni kuongoza Kamati hiyo ya Bunge, alisema licha ya kuanza vyema yapo mambo ambayo hayakumridhisha katika bajeti.

“Lazima tufanye matumizi ya kawaida kwa kutumia mapato ya ndani. Hili tulilizungumza katika Kamati yetu wakati wa mashauriano na Serikali. Lakini tulisema kwa kuwa Waziri ni mgeni, ndio kwanza ameteuliwa, tumpe muda, ajipange hadi bajeti ya 2013/14,” alisema Chenge.

Alisema ni vyema pia sekta binafsi ikawekewa mazingira mazuri ili kushawishi ukuaji wa uchumi; huku akieleza kwamba tayari kampuni za bia na sigara zimeeleza kusikitishwa na ongezeko la bei katika bidhaa zao.

Kuhusu kilimo, alisema lazima Serikali isaidie kuweka miundombinu bora ya kilimo na kuhakikisha barabara zinapitika wakati wote ili wakulima waweze kutoa mazao yao mashambani na kuyapeleka sokoni.

Alisema si hivyo tu, bajeti inapaswa kulenga watu wa vijijini ambako ndiko waliko asilimia kubwa ambao ni wakulima, ili kuzalisha kwa wingi na kuiwezesha nchi kuwa na uchumi imara.

Mbunge wa Simanjiro, Christopher ole Sendeka (CCM), alisema baadhi ya maeneo, Serikali haijafanya vizuri katika bajeti ikiwamo kutoa nafuu ya kodi kwa kampuni kubwa zikiwamo za madini.

Alisema unafuu huo wa kodi haufai kwa kampuni na viwanda vikubwa, wakati wanapaswa kulipa kodi kubwa.

Aidha, Sendeka alilalamikia kiwango kidogo kilichotengwa kwa umeme, Sh bilioni 400, akisema hazitoshelezi kwa sababu ya gharama kubwa za kukodi mitambo ya kuzalisha umeme zinazobebwa na Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco).

Kiongozi wa Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe, alitaka Serikali itaje kiasi cha mishahara kilichoongezwa, badala ya kuachiwa waziri wa kisekta, kwa sababu hilo ni moja ya maeneo yanayohitaji uzito.

Aidha, alilalamikia matumizi kuwa makubwa, kutofutwa kwa posho, mfumuko wa bei akisema umejikita katika kuagiza chakula nje na kuanzisha kilimo cha umwagiliaji katika mabonde makubwa nchini.

Mbunge wa Kigoma Kaskazini ambaye pia ni Naibu Kiongozi wa Upinzani Bungeni,  Kabwe Zitto alisema bajeti hiyo imejikita zaidi katika mikopo na madeni.

Katika hotuba yake ya Bajeti, Dk Mgimwa alisema katika bajeti hiyo yenye kubeba Sh trilioni 15, asilimia 70 itakuwa kwa matumizi ya kawaida na asilimia 30 kwa matumizi ya maendeleo.

Wakati hayo yakijiri, wabunge wa CCM walikuwa na kikao jana asubuhi; na miongoni mwao walieleza kutoridhishwa ni kutofutwa kwa Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) katika malighafi za viwanda vya nguo na mavazi.

Mmoja wa wabunge hao wa CCM, alieleza kuwa licha ya Waziri Mkuu Mizengo Pinda kuunda kamati maalumu ya wadau wa sekta ya pamba na viwanda vyake, mapendekezo ya kamati hiyo hakuyazingatiwa katika bajeti.

Mapendekezo yalikuwa ni viwanda kupewa msamaha wa VAT kwenye bidhaa za nguo na mavazi, na ilielezwa kuwa hilo linawezekana kwa sababu kiwango kinachokusanywa sasa ni karibu Sh bilioni moja kwa mwaka.

Advertisements
 
Leave a comment

Posted by on June 17, 2012 in Tanzania News

 

Tags: , , , , , ,

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out / Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out / Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out / Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out / Change )

Connecting to %s

 
%d bloggers like this: